Jumanne 14 Aprili 2026 - 09:20
Ataba ya Abbas (as) yaitikia wito wa Ayatullah Sistani katika kutoa misaada kwa Iran na Lebanon

Hawza / Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad al-Safi alisisitiza kwamba; watu wa Iraq wana uhusiano wa kipekee na Mtukufu Ayatullah Sistani, na wanaonesha mwitikio chanya katika miongozo yake ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad al-Safi, msimamizi wa kisheria wa Ataba Tukufu ya Abul-Fadhl al-Abbas (as) na mwakilishi wa Ayatullah Sistani, katika hafla ya kupokea “Tajammu‘ al-Ghayrah al-Husayniyyah” kutoka mji wa Za‘faraniyah ambao upo ndani ya mji mkuu Baghdad, alisisitiza kwamba; watu wa Iraq wana uhusiano wa kipekee na Ayatullah Sistani na wana mwitikio chanya kwenye miongozo yake ya kibinadamu.

Katika mkutano huu, alisikiliza kwa kina maelezo ya mkusanyiko huo kuhusu juhudi za kukusanya misaada kwa ajili ya kuyaunga mkono mataifa mawili ya Iran na Lebanon.

Mwakilishi wa Ayatullah Sistani katika mkutano huo alisema kuwa; watu wa Iraq wana uhusiano wa kipekee na Ayatullah Sistani, na wana mwitikio chanya kwenye miongozo inayotolewa na yeye; kama vile wito wa kutoa msaada kwa wakimbizi katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi ya Daesh, kuunga mkono wapiganaji na familia za mashahidi, kusaidia walioathirika katika kipindi cha janga la corona, na pia msaada wa awali kwa mataifa ya eneo baada ya tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria, pamoja na kuunga mkono watu wa Palestina na Lebanon katika migogoro ya kibinadamu.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Safi aliongeza: Mataifa yaliyoathirika yanaposhuhudia mwitikio wa watu wa Iraq katika kutoa misaada ya chakula na dawa, hupata faraja ya kiroho na kuhisi mshikamano, na jambo hili si geni kwa watu wetu wakarimu. Yeyote anayekuja Iraq katika siku za Arbaeen ataona ukarimu huu wa kipekee. Aidha, watu wa Iraq wanaamini kuwa mali na juhudi hizi zitalipwa kwa wamiliki wake kwa mara dufu zaidi.

Msimamizi wa kisheria wa Haram ya Abbas (as) alisisitiza kuwa: Jambo hili si la ajabu kwa watu wa Iraq; kwa sababu wao katika vipindi vingi vya historia wamepitia hali ya uhitaji, na wanahisi maumivu ya wahitaji na waliofiwa. Sifa za ukarimu na kujitolea zimekua ndani yao katika nyakati zote na zimewafanya kuwa mfano katika utoaji; kwa sababu wamelelewa katika shule ya Imam Hussein (as).

Alisema: Roho hii ya mshikamano inaharakisha kudhihiri kwa Mola wetu, Sahib al-‘Asr wa al-Zaman (aj). Na aliutakia ugeni huu tawfiq na msaada wa Mwenyezi Mungu katika kila jambo lenye kheri.

Kwa upande mwingine, Sheikh Saif al-Rikabi, mwanachama wa “Tajammu‘ al-Ghayrah al-Husayniyyah”, alisema: Leo tumepata heshima kubwa ya kukutana na mwakilishi wa Ayatullah Sistani, Sayyid Ahmad al-Safi.

Aliongeza: Sisi tangu mwaka 2014 (1392 Hijria Shamsia), tangia wakati Ayatullah Sistani alipotoa wito wa kusaidia wakimbizi waliotokana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi ya Daesh dhidi ya Iraq, tumekuwa tukifanya kazi katika njia hii; pia katika kipindi cha janga la corona. Na bado tunaendelea na kazi katika njia ya miongozo yake.

Sheikh al-Rikabi aliendelea: Sisi kila siku tunajifunza kutoka kwa watoaji misaada. Baadhi ya watoto walibeba mabango yenye ujumbe wa kuahirisha sherehe zao za siku ya kuzaliwa hadi siku ya kutangazwa ushindi, na baadhi ya wanawake walitoa pete zao za ndoa kwa ajili ya kuunga mkono watu wa Lebanon na Iran.

Inafaa kutajwa kwamba; Ataba
Tukufu ya Abbas (as), kwa kuitikia wito wa Ayatullah Sistani, imeanzisha kampeni kubwa ya kibinadamu kwa ajili ya kuunga mkono mataifa mawili ya Iran na Lebanon.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha